Wednesday, 26 April 2017

ATHARI ZA MAAMBUKIZI KATIKA MIRIJA YA UZAZI


TATIZO hili kitaalamu hutamkwa ‘Salpingitis’, ni maambukizi ndani ya mirija ambayo huathiri na kuleta mabadiliko yasiyotarajiwa katika mirija hiyo.
Tatizo hili huambatana na hali ya maambukizi katika viungo vya uzazi au ‘PID’.
Maambukizi katika mirija ni matokeo ya kusambaa kwa maambukizi haya toka ukeni, katika kuta za kizazi hadi kwenye mirija na vifuko vya mayai.
Maambukizi yakiwa makali na ya muda mrefu husambaa nje ya kizazi na kusababisha tatizo liitwalo ‘Pelvic Perisoneum.
Maambukizi katika mirija ya uzazi yapo katika makundi mawili, kwanza Acute ni yale sugu ‘Chronic Salpingitis’ na pili ni yale makali ‘Chronic Salpingitis’, maambukizi haya hutokea kwa vipindi tofauti kutokana na ukali wa ugonjwa.
Dalili za ugonjwa
Dalili hizi hujitokeza zaidi baada ya kumaliza damu ya hedhi, dalili ni kama vile kutokwa na hali ya uchafu usio wa kawaida ukiwa na harufu mbaya, uchafu huu unaweza kuwa na rangi ya njano au ya damu. Pia maumivu wakati ukiwa kwenye upevushaji mayai ‘Ovulation pain’, maumivu makali wakati wa hedhi ambapo hapo awali hayakuwepo, maumivu chini ya tumbo muda wote yakiambatana na maumivu ya kiuno.
Hali ikiwa mbaya mgonjwa hupata kichefuchefu, hutapika, huhisi homa kila wakati, mwili kutokuwa na hali nzuri huku tumbo likiuma na uchafu ukiendelea kutoka ukeni ukiambatana na harufu mbaya. Mgonjwa pia hulalamika muwasho au maumivu ukeni na wakati mwingine huhisi maumivu anapokojoa.
 Kama tulivyoona, maambukizi haya huanzia ukeni na husambaa hadi katika viungo vingine kwa ndani.
Athari za tatizo
Maambukizi yanaweza kusambaa hadi katika mirija toka ukeni hadi ndani ya kizazi pale mwanamke anapokuwa katika damu ya hedhi na kama damu itarudi kwa juu, hii siyo hali ya kawaida na tutakuja kuiona katika makala zijazo. Matatizo mengine yanayoweza kusababisha hali hii ya maambukizi ni usafishaji wa kizazi mara kwa mara na uharibikaji wa mimba.
Magonjwa yaenezwayo kwa ngono pia ni tatizo kubwa katika uharibifu wa mirija.
Bakteria wanaosababisha tatizo hili la maambukizi na uharibifu wa mirija ni ‘Neisseria Gonorrhea’ ambayo husababisha ugonjwa wa kisonono au gono.
Kwa ujumla ugonjwa huu husababishwa na aina nyingi ya vijidudu vya bakteria.
Ugonjwa huu hushambulia viungo vya uzazi vya mwanamke ambako mimba hutungwa. Huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa hasa umri wa kuanzia miaka 15-35.
 Wanawake wengi huwa hawapati dalili za awali za ugonjwa, dalili zinapojitokeza tatizo hili huchangia wanawake wengi kutafuta tiba kwa muda mrefu na wengi hukusanyika katika kliniki za magonjwa ya kinamama.
Mirija ya mayai inaposhambuliwa na ugonjwa husababisha kuziba hivyo humfanya mwanamke apoteze uwezo wa kuzaa au ikitokea akapata mimba basi itakuwa nje ya kizazi.
Nini cha kufanya?
Ni vema mwanamke awahi hospitali kufanyiwa uchunguzi pale anapohisi kuna hali isiyo ya kawaida ukeni na chini ya tumbo ambayo inaendelea kwa muda mrefu.
Epuka matatizo au vyanzo mbalimbali vya maambukizi ukeni katika kizazi.
Katika makala zilizopita tumezungumza mengi kuhusu uchunguzi na tiba ya kuziba mirija.
 Ni muhimu wewe kuanza kufuatilia hospitali za mikoa kwa uchunguzi na tiba.

No comments:

Post a Comment

MAWASILIANO.

MAWASILIANO. SIMU NO. +255 713 684 712 E-MAIL: healthylivingproduct6@gmail.com TUPO : KUNDUCHI BAHARI BEACH