Wednesday, 26 April 2017

MAAMBUKIZI YA TEZI DUME (PROSTATITIS) SEHEMU YA PILI

Maambukizi ya tezi dume bila uwepo wa bakteria (Chronic non-bacterial prostatitis)

Kama jina lake linavyoeleza, maambukizi ya aina hii kwenye tezi dume husababishwa na msongo wa mawazo, matatizo katika vichocheo vya mwili
 (homoni) na hata matatizo katika mfumo mzima wa neva.Pia kumekuwepo na dhana ya kwamba maambukizi ya aina hii huchangiwa na kuwepo kwa

maumivu ya kibofu cha mkojo yanayotokana na maambukizi katika kibofu hicho 
(Cystitis)au hali ya hewa hususan baridi ambayo huongeza maumivu ya tezi dume na hali ya joto ambayo hupunguza maumivu hayo. Baridi pia huchangia kujirudia kwa dalili na viashria vya maambukizi haya.

Katika utafiti uliofanyika kaskazini mwa nchi ya 
Finland (nchi ambayo ina majira ya baridi kali sana),umeonyesha ya kuwepo kwa maambukizi ya aina hii yanayoambatana na dalili na viashiria vyake kali sana kuliko sehemu yoyote duniani.
Maambukizi haya ya tezi dume bila uwepo wa bakteria hutokea kwa wanaume walio katika umri wa miaka 35-45 na inakisiwa kutokea kwa asilimia 90-95 ya maambukizi yote ya tezi dume .

Kuna aina mbili kuu za maambukizi haya ambazo ni:

1.Maambukizi haya yanayoambatana na mcharuko 
(Inflammatory Chronic Prostatitis/Chronic Pelvic Pain Syndrome)
2.Maambukizi yasiyokuwa na mcharuko 
(Non-infalmmatory chronic prostatitis, CP/Chronic Pelvic Pain Syndrome au CPPS)

Nini hasa hutokea wakati wa maambukizi haya?

Kukosekana kwa udhibiti wa mfumo wa neva mwilini kutokana na kuwepo kumbukumbu za maumivu yoyote 
(past trauma), maambukizi kwenye tezi dume, mrundikano wa kemikali tofauti tofauti na kuwepo kwa hali ya kuvutika kwa neva za kwenye nyonga husababisha mcharuko (inflammation) 

katika tezi dume unaosababishwa na kutolewa kwa wingi kwa kemikali aina ya substance P
(kutoka kwenye msihipa ya neva)ambayo ndio husababishwa kutolewa chembechembe zinazosababisha mcharuko mwili (mast cells) kwa wingi na matokeo yake ni kuathiri tezi dume pamoja na viungo vilivyokaribu yake kama kibofu cha mkojo, mpira wa kupitisha mkojo (urethra),korodani nk.

Dalili na viashiria vya maambukizi ya tezi dume bila uwepo wa bakteria
•Maumivu makali ya kwenye sehemu za siri au kwenye nyonga kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu bila kuwepo kwa maambukizi ya mfumo wa mkojo 
(UTI)
•Maumivu haya makali yanaweza kuenea hadi kwenye mgongo kwa chini, kwenye puru 
(rectum) na kumfanya mgonjwa kushindwa kukaa chini/ kwenye kiti.
•Maumivu wakati wa kukojoa
•Maumivu katika jointi za mifupa
•Maumivu ya misuli 
(myalgia)
•Maumivu ya tumbo
•Uchovu usioelezeka
•Kichomi kwenye uume/dhakari 
(constant burning pain in the penis)
•Maumivu ya mara kwa mara kwenye nyonga, korodani au kwenye puru 
(rectum) bila uwepo wa maambukizi kwenye kibofu cha mkojo
•Maumivu wakati wa kutoa shahawa (wakati wa kujamiana)
•Kukojoa mara kwa mara
•Maumivu baada ya kutoa shahawa (baada ya kujamiana) ni dalili kubwa ya maambukizi haya
•Kupungua hamu ya kufanya mapenzi
•Kushindwa kujamiana vizuri 
(sexual dysfunction)
•Kushindwa kusimika/kudisa (jogoo kushindwa kupanda mtungi)Erectile dysfuction


Vipimo vya uchunguzi
Hakuna kipimo maalum cha kuchunguza maambukizi haya ya tezi dume.

Vipimo vinavyoweza kusaidia katika uchunguzi wa maambukizi haya ni pamoja na 

•kipimo cha kuangalia shahawa 
(semen analysis)
•kipimo cha kuangalia wingi wa cytokines kutoka kwenye majimaji ya tezi dume
•Vipimo vya kuangalia viashiria vya mcharuko
(inflammation) kama cytokines,myeloperoxidases na chemokines
Inflammatory 
CP/CPPS huambatana na kuwepo kwa seli za usaha (pus cells) kwenye mkojo, shahawa na kwenye majimaji ya tezi dume wakati Non inflammatory CP/CPPS haina seli hizi za usaha kwenye mkojo, shahawa na majimaji ya tezi dume.Kielezo hiki si kigezo cha kutumika kama kipimo cha kuchunguza maambukizi haya.
Seli za usaha (pus cells) huwa ni chembechembe za damu nyeupe zilizokufa.

Matibabu ya maambukizi ya tezi dume bila uwepo wa bakteria
Maambukizi haya sio rahisi kutibu kwani hakuna tiba maalum inayokubalika na wataalamu wa afya.
Lengo kuu la matibabu ya maambukizi haya ni kupunguza mvutano unaosababishwa na kuvutika kwa misuli ya nyonga na ya kwenye puru ,

kupunguza msongo wa mawazo na vichangizi vya msongo huu wa mawazo.

Miongoni wa matibabu yanaweza kusaidia ni pamoja na:
•Kujua chanzo cha msongo wa mawazo/wasiwasi
(panic disorder) au taharuki na kumsaidia mgonjwa kuepuka vichagizi hivi
•Ushauri nasaha pamoja na kumhakikishia mgonjwa ya kwamba hali yake itatengemaa
•Kumuona daktari wa magonjwa ya akili
•Kufanya mazoezi ya yoga ili kufanya nyoga pamoja na mishipa ya neva ya nyoga na misuli kuwa katika hali tulivu
(relaxation)
•Massage ya tezi dume 
(Digital prostate massage)
•Mazoezi ya viungo kwa wale ambao bado hawajafikia hatua ya kupata maumivu makali 
(Chronic Fatigue Syndrome)
•Dawa za kupunguza msongo wa mawazo kama antidepressants, benzodiazipines nk.
•Dawa za antibiotiki na alpha blockers hazijatoa matokeo ya kuridhisha katika uponyaji wa maambukizi haya
•Tiba ya acupuncture imeonyesha kuwapa unafuu baadhi ya wagonjwa

Wanaume wenye maambukizi haya ya tezi dume wako kwenye hatari ya kupata tatizo la maumivu makali sana 
(Chronic fatigue syndrome) na ugonjwa wa Irritable Bowel Syndrome( unaoambatana na maumivu ya tumbo, tumbo kuwa kubwa, kuharisha mara kwa mara au kutopata haja kubwa, msongo wa mawazo, wasiwasi, kuharisha damu na nk)

No comments:

Post a Comment

MAWASILIANO.

MAWASILIANO. SIMU NO. +255 713 684 712 E-MAIL: healthylivingproduct6@gmail.com TUPO : KUNDUCHI BAHARI BEACH