Wednesday, 26 April 2017

LISHE BORA KWA MTOTO























Huwa ni furaha kubwa katika familia mtoto anapozaliwa, na hata katika tamaduni fulani fulani sherehe kubwa hufanyika kumkaribisha mwanafamilia mpya aliyezaliwa. Lakini pamoja na familia kuwa katika hali ya furaha, wazazi wa mtoto aliyezaliwa huwa na maswali mengi ya kujiuliza. Tutamleaje mtoto ili awe mwanajamii mwenye tabia njema? Lishe ya mtoto wetu iweje ili akue akiwa mwenye afya njema ya mwili na akili? Tutamwepushaje mwanetu na maradhi haya yanayotishia maisha ya watoto?. Katika hali ya kutafuta majibu ya maswali haya, wazazi hujikuta katika kila aina ya sintofahamu
kutokana na ushauri mbalimbali waupatao kuhusu lishe au malezi ya watoto wao.

Sayansi ya afya inatoa ushauri  ambao utasaidia wazazi wapya kuwa na mwanzo mzuri wa lishe ya mtoto ili akue akiwa na afya njema. Katika maisha, jinsi vile tunavyoanza, yaweza kutabiri jinsi vile tutakavyomaliza. Hii inaamaanisha kuwa lishe bora kwa mtoto katika nyakati zake za mwanzo wa maisha yake, ni muhimu sana kwa afya ya baadae katika maisha yake. Tafiti zinaonyesha kuwa, lishe bora kwa binadamu katika utoto wake, huchangia sana kuwa na maisha mazuri baadae, kufanya vizuri shuleni, kazini na hata jinsi anavyoweza kushirikiana na jamii inayomzunguka. Pia aina bora ya vyakula tutakavyokula tukiwa wachanga, vitatusaidia baadae maishani kuwa na miili yenye nguvu na afya, kinga ya mwili iliyo imara na kuwa na umri mrefu wa kuishi.

Chakula muhimu sana kwa mtoto mchanga katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yake ni maziwa ya mama. Maziwa ya mama ni yenye lishe ya hali ya juu, yenye mchanganyiko maalum wa virutubisho na kinga kutoka kwa mama kwa ajili ya mtoto.Vitu muhimu vilivyomo katika maziwa haya ni kinga ya mwili(antibodies), vijidawa (antimicrobial factors), vimeng’enyo, vitamini, madini muhimu, mafuta na protini (vyote hivi husaidia ukuaji wa haraka wa mwili na ubongo wa mtoto).

Watoto huanzishiwa lishe ya vyakula vingine wanapokua na umri wa angalau miezi 4 hadi 6, kwa kuwa watoto wachanga huwa hawawezi kumeng’enya aina nyingi za vyakula. Kwa kawaida watoto huanzishiwa vyakula hivi pale uzito wao wa mwili unakuwa mara mbili ya uzito waliozaliwa nao, na hii ni endapo wanaweza kukaa, shingo imekuwa na nguvu, wanaweza kufungua mdomo wanapopewa chakula na wanaweza kumeza vyakula laini, mara nyingi huweza kufanya hayo yote wakiwa na miezi sita.

Vyakula hivi wanavyoanzishiwa watoto huwa ni nyongeza ya maziwa ya mama na siyo mbadala wa maziwa ya mama. Chakula  cha mwanzo cha mtoto ni lazima kiwe cha maji maji na laini.Pata msaada wa kujua ni wakati gani hasa wa kumuanzishia mtoto vyakula, wasiliana na wataalamu au wauguzi katika cliniki mtoto anayoudumiwa. Usimwanzishie mtoto aina nyingi za vyakula kwa wakati mmoja ila umwanzishie chakula kimoja hadi kingine kwa nyakati tofauti na uchunguze endapo kama kuna chakula chenye kumletea mtoto aleji. Usimwanzishie mtoto vyakula kama mayai, asali, karanga au siagi ya karanga na aina nyinginezo na nati kwa sababu vyakula hivi ni rahisi kusababisha aleji, asali yaweza kuwa na vijimelea vya bakteria vilivyolala( kwa kitaalam hujulikana kama endospores) ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi kwa watoto wachanga kwa kuwa kinga yao ya mwili bado haijaimarika.

Tunapowaanzishia vyakula  watoto wachanga, lazima tufuate mtiririko ufuatao; hatua ya kwanza ni kuanza na vyakula vya nafaka kama uji wa mchele au mahindi. Vyakula hivi huendana na mwili wa mtoto na ni nadra sana mtoto kuwa na aleji ya vyakula hivi.

Hatua ya pili ni kumuanzishia mtoto vyakula vya mboga mboga.Vyakula hivi huwa na virutubisho vingi zaidi ya matunda yenye sukari nyingi. Vyakula hivi vya mboga mboga ni kama viazi vitamu, bitiruti,maboga na karoti ambavyo ni rahisi kupika na kuviponda ponda kutengeneza chakula laini cha mtoto.

Hatua ya tatu ni kuanza kumpa mtoto vyakula kutokana na matunda. Watoto wanaoanzishiwa matunda kabla ya kuanzishiwa mboga mboga, hujijenga katika akili yao kuwa vyakula ni vyenye ladha ya sukari na wanapoanzishiwa mboga mboga itakuwa vigumu kwao kuzoea ladha yake. Sababu nyingine ni kwamba wanakuwa bado hawana uwezo wa kumeng’enya  sukari iliyo katika matunda aina ya fructose ipasavyo.Unaweza kumuanzishia matunda kwa kumpa ndizi mbivu iliyopondwa pondwa na kumchanganyia na maziwa ya mama. Waweza kumpa pia matunda yaliyopikwa kama tipisi, peasi au epo.

Hatua ya nne ni kumuanzishia mtoto vyakula vya protini.Vyakula hivi ni kama maharagwe yaliyopondwa pondwa pia dengu, njegere za kijani na nyama iliyosagwa. Kwa kuwa tumbo la mtoto linakuwa bado halijaweza kumeng’enya vyakula hivi vizuri, waweza kuviona vikitoka katika choo cha mtoto vikiwa kama alivyokula. Hii inapotokea usiwe na wasiwasi, kwa kuwa hali hiyo itatoweka kadri mtoto anavyoendelea kuvizoea vyakula hivyo.

 Watoto zaidi ya mwaka 1 zingatia mlo kamili wenye makundi yote ya chakula. Mtoto anapokula aina tofauti za vyakula hukamilisha mlo kamili. Mlo kamili utamsaidia mwanao kupata aina zote za virutubisho anavyovihitaji. Kuwa mbunifu ili kugundua aina ya chakula mtoto akipendacho.Wakati mwingine watoto wanapopewa chakula kwa mara ya kwanza huwawia vigumu kuikubali ladha ya chakula hicho, lakini baada ya muda fulani tunapoendelea kuwapa chakula hiki hujifunza na kujikuta wamezoea ladha ya chakula hicho. Kama mtoto hatopenda kula yai la kuchemsha jaribu kumpa maziwa, na kuendelea kubadili vyakula kadiri mtoto anavyopendelea. Ubunifu wa aina za chakula na ubadilishaji kulingana na chakula akipendacho, utaondoa tatizo la mtoto kukataa kula. Mfano, chakula kama nyama kitamwongezea mtoto protini, lakini anaweza pia kupata protini kutoka katika nati, maharagwe,dengu na njegere.

Ili kumsaidia mtoto aondokane na tatizo la kukataa kula, mpe aina mbali mbali za vyakula kutoka katika makundi yafuatayo.
Vyakula vya wanga
  • Viazi mviringo au viazi vitamu.
  • Nafaka kama mahindi, mchele, ngano na nyinginezo.
  • Majimbi na ndizi.

Nafaka zisizokobolewa huwa na kiasi kikubwa cha fiba ambazo zina aina nyingi za virutubisho.Kuwa makini na kiasi unachompa mtoto kwa kuwa nafaka hizi zisizokobolewa hushibisha sana na kumpa kwa wingi kutasababisha mtoto kuvikataa vyakula hivi. Kumbuka tumbo la mtoto ni dogo na ni kiasi kidogo kitakachomfanya ashibe.

Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma na protini.
Mtoto anahitajika kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma na protini mara mbili kwa siku.Vyakula hivi ni kama:
  • Nyama.
  • Samaki.
  • Nati.
  • Mayai.
  • Njegere,maharagwe na dengu.
Hakikisha  unanunua nyama yenye ubora kutoka katika bucha zenye nyama iliyopimwa.Epuka kununua nyama kutoka wauzaji wa mitaani ili kumwepusha mtoto na magonjwa hususani ugonjwa hatari kama kimeta. Kama utapendelea kumpa mtoto vyakula aina ya nati(karanga,kweme,korosho,nazi na nyinginezo) hakikisha zimesagwa na kumchanganyia katika chakula chake ili kuepuka mtoto kukabwa.

Vyakula kutokana na maziwa.
  • Maziwa.
  • Jibini.
  • Mtindi (yoghurt)
Kama utapenda kumpa mtoto mtindi, chagua ule usiowekewa ladha na usio na sukari nyingi. Kama utapenda kuongeza ladha, fanya hivyo kwa kuchanganya na matunda yenye ladha azipendazo mtoto. Maziwa ni chanzo kizuri cha madini ya kalshamu (calcium). Hakikisha mtoto wako anapata kiasi cha nusu lita ya maziwa kwa siku. Madini haya ni muhimu kwa kuwa huimarisha mifupa,meno na muhimu kwa utendaji kazi wa misuli. Watoto wenye upungufu wa madini haya hupatwa na ugonjwa ujulikanao kama rickets ambao husababisha udhaifu wa mifupa ambayo hupinda na kusababisha matege. Hakikisha mtoto wako anatumia maziwa yasiyoondolewa siagi kwa kuwa watoto wanahitaji nishati nyingi ya mwili ili wakue. Pia maziwa haya yasiyoondolewa siagi huwa na kiwango kikubwa cha Vitamini A.

Matunda na mboga za majani.
  • Embe,chungwa ,zabibu na nanasi.
  • Tikiti maji.
  • Parachichi.
  • Papai.
  • Karoti.
  • Mboga za majani.
Matunda ni muhimu kwa watoto kwa kuwa huwaongezea aina mbalimbali za vitamini muhimu zinazohitajika mwilini. Jaribu kubadilisha aina za matunda kulingana na ladha aipendayo mtoto.

Vyakula vinavyohitajika kwa kiasi.
Vyakula vyenye mafuta mengi na sukari nyingi ni kama siagi, mafuta ya mimea, keki,chokleti,chipsi, biskuti, pipi na vinywaji kama soda.Miili ya watoto huitaji kiasi kikubwa cha nishati, lakini kuwapa kiasi kikubwa cha vyakula hivi kwaweza kusababisha kuwa na uzito mkubwa(obesity). Endapo utachagua kumpa vyakula hivi, hakikisha anakula kiasi kidogo na ikiwezekana ale vyakula hivi kwa vipindi mfano wakati wa sikuu ya kuzaliwa au siku za mwisho wa wiki pekee.Ni vizuri tahadhari kuchukuliwa kwa kuwa vyakula vyenye sukari nyingi huweza pia kusababisha magonjwa ya kuoza kwa meno.

Watoto hawaitaji kula vyakula vyenye chumvi nyingi. Epuka vyakula vya migahawani ambavyo huwa na chumvi nyingi.

Kama mtoto ana tatizo la pumu, aleji ya chakula au kuna historia ya aleji katika familia,epuka kumpa chakula kama karanga kabla ya kuonana na mtaalam wa lishe au daktari ili kuweza kuzuia madhara anayoweza pata mtoto.

No comments:

Post a Comment

MAWASILIANO.

MAWASILIANO. SIMU NO. +255 713 684 712 E-MAIL: healthylivingproduct6@gmail.com TUPO : KUNDUCHI BAHARI BEACH