Wednesday, 26 April 2017

KUVIMBA KWA TEZI DUME (BENIGN PROSTATE HYPERPLASIA BPH) FEATURE




Tezi Dume (Prostate gland)

Tezi dume ni sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa kiume. Inaundwa na sehemu mbili, lobes, ambazo zimeunganishwa na kufunikwa kwa nje kwa utando wa tishu. Tezi hii ipo mbele kidogo ya puru (rectum) na na chini kidogo ya kibofu cha mkojo. Tezi dume inauzunguka mrija unaounganisha kibofu cha mkojo na uume (urethra).

Mojawapo ya kazi za tezi dume ni kutoa majimaji yanayochanganyika na mbegu za kiume (sperms) wakati wa kilele cha tendo la ngono. Mchanganyiko huu wa mbegu pamoja na majimaji hayo hufanya shahawa (semen). Aidha majimaji hayo husaidia kuzipa mbegu za kiume nguvu ya kusafiri kwenye uke mpaka kufikia kwenye mirija ya fallopian tayari kwa utungisho na yai la kike. Vilevile husaidia kupunguza hali ya kitindikali iliyopo katika uke, ambayo kama isiporekebishwa, huweza kuua mbegu nyingi za kiume na kufanya utungisho kuwa wa tabu.


Kuvimba Tezi Dume (BPH)



Kwa kadiri mwanaume anavyozeeka, ni jambo la kawaida pia kwa tezi dume kuongezeka ukubwa na kuvimba. Hali hii kitabibu huitwa Benign Prostate Hyperplasia au wengine hupenda kutumia maneno Benign Prostate Hypertrophy kwa kifupi BPH. Kwenye makala hii tutautumia sana ufupisho huu wa BPH ili kurahisisha mambo.
Ukuaji wa tezi dume hupitia hatua kuu mbili. Hatua ya kwanza hutokea kipindi cha balehe wakati tezi dume linapoongezeka ukubwa na kuwa mara mbili ya lilivyokuwa hapo awali. Baada ya hapo ukuaji husimama kwa muda mpaka kijana anapofikisha miaka 25 hadi 30 ndipo hatua ya pili ya ukuaji huanza tena. Ukuaji huendelea kwa viwango na kasi tofauti kati ya mtu na mtu na hatimaye kusababisha BPH katika umri wa utu uzima.
Wakati tezi dume linapokua na kutanuka, utando wa tishu unaozulizunguka hutanuka pia. Hata hivyo ingawa tezi dume huendelea kukua, hufikia wakati utando wake huacha kutanuka na kufanya tezi dume kubana mrija wa kutolea mkojo kutoka kwenye kibofu. Hali hii husababisha kibofu cha mkojo kuwa na ngozi ngumu. Hali hii hufanya kibofu cha mkojo kuhisi kutaka kutoa mkojo nje hata kama kiasi cha mkojo ndani yake ni kidogo sana. Hufikia wakati, kibofu huwa dhaifu na kupoteza uwezo wake wa kuhisi kutoa mkojo na hivyo kufanya mtu anapokojoa kushindwa kutoa mkojo wote na badala yake hubakiza kiasi fulani cha mkojo kwenye kibofu.

BPH husababishwa na nini?
Chanzo halisi cha BPH au vihatarishi vyake (risk factors) havijulikani kwa uhakika. Kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa kuwa BPH hutokea kwa wanaume watu wazima na wazee tu. Aidha imewahi kuonekana huko nyuma kuwa PBH haitokei kwa wanaume ambao wamewahi kufanyiwa operesheni ya kuondoa korodani au wale ambao walizaliwa bila korodani. Hali imepelekea baadhi ya watafiti kuamini kuwa BPH ina uhusiano mkubwa na umri wa mtu pamoja na uwepo wa korodani.
Kuna dhana (theories) kadhaa zinazojaribu kuelezea chanzo cha BPH. Dhana hizo ni pamoja na


  1. Uhusiano kati ya BPH na homoni ya estrogen: Wanaume huzalisha testosterone, homoni ya muhimu sana katika mwili wa mwanaume. Hali kadhalika huzalisha pia estrogen ambayo ni homoni ya kike kwa kiwango kidogo sana. Kadiri jinsi mtu anavyozeeka, ndivyo uzalishaji wa testosterone unavyokuwa mdogo na kufanya kiwango chake katika damu kupungua kulinganisha na kiwango cha estrogen ambacho huongezeka kwa kiasi fulani. Pamoja na kazi nyingine, estrogen pia huchochea ukuaji wa chembe hai za mwili. Tafiti zilizofanywa kwa wanyama zimeonesha kuwa BPH hutokea kwa sababu kiwango kikubwa cha estrogen katika damu huchochea ukuaji wa seli za tezi dume na hivyo kufanya tezi dume kuvimba.
  2. Uhusiano kati ya BPH na Dihydrotestosterone (DHT): DHT ni kiasili kinachozalishwa kutokana na testosterone kwenye tezi dume, ambacho husaidia kuthibiti ukuaji wa tezi dume. Ingawa wanyama wengi hupoteza uwezo wa kuzalisha DHT wanapofikia umri wa uzee, baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa, kwa binadamu, hata kama kiwango cha testosterone kitapungua sana katika damu, wanaume watu wazima bado wana uwezo wa kuzalisha kiasili hiki cha DHT katika tezi dume zao. Uzalishaji na uklimbikaji huu wa DHT huchochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa seli za tezi dume na kusababisha BPH. Wanasayansi wamegundua kuwa wanaume watu wazima wenye kiwango kidogo cha DHT hawapati BPH.
  3. Uhusiano kati ya BPH na maelekezo ya seli: Dhana nyingine inasema kwamba baadhi ya seli kutoka katika sehemu fulani ya matezi yanayohusika na ukuaji mwilini hupewa maelekezo wakati mtu anapokuwa bado mdogo. Seli hizi hutunza maelekezo hayo na baada ya miaka kadhaa maelekezo haya huanzwa kutekelezwa na seli za matezi mengine. Mojawapo ya melekezo hayo ni kuchochea ukuaji wa tezi dume na kusababisha BPH.


Dalili za BPH
Dalili za BPH hutokea kwa sababu ya kubanwa kwa njia ya kutoa mkojo nje ya mwili (urethra) au kibofu kushindwa kuthibiti mkojo. Aidha dalili hizi hutofautiana kati ya mtu na mtu, ingawa karibu wagonjwa wote 


  1. Hukojoa mkojo unaokatika katika
  2. Hukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu
  3. Husita kabla ya kuanza kukojoa
  4. Hali ya kujihisi kubanwa na mkojo kila mara
  5. Kushindwa kuthibiti mkojo kiasi cha mkojo kutirika wenyewe
  6. Hali ya kuhisi mkojo haujaisha kwenye kibofu
  7. hukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku
  8. Kushindwa kukojoa kabisa (urine retention)
  9. Au dalili zinazotokana na madhara ya BPH


Madhara ya BPH
BPH kama ilivyo saratani ya tezi dume, inaweza kumletea mgonjwa madhara (complications) kadhaa. Madhara hayo ni pamoja na 



  1. Mkojo kushindwa kutoka (retention of urine)
  2. Mgandamizo kwenye kibofu cha mkojo
  3. Vijiwe kwenye kibofu cha mkojo
  4. Uambukizi katika njia ya mkojo (UTI)
  5. Madhara katika figo au kibofu
  6. Shinikizo la damu
  7. Kushindwa kutoa shahawa kwenye uume (retrograde ejaculation)
  8. Maambukizi mbalimbali
  9. Nimonia (Pneumonia)
  10. Damu kuganda
  11. Uhanithi


Vipimo na Uchunguzi

Baada ya mgonjwa kujihisi dalili zilizotajwa hapo juu, daktari atamfanyia uchunguzi wa mwili kabla ya kumfanyia vipimo zaidi. Vipimo vyaweza kutofautiana kati ya mgonjwa namgonjwa, lakini baadhi ya vipimo ni pamoja na


  1. Kuchunguza Tezi Dume kupitia njia ya haja kubwa au Digital Rectal Examination (DRE): Hiki ni kipimo cha kwanza kabisa ambacho mgonja hufanyiwa na daktari wake. Ni kipimo kinachoweza kumpa daktari picha ya tatizo na kufahamu kuhusu ukubwa na hali ya tezi dume. Daktari akiwa amevaa glovu huingiza kidole chake cha shahada katika njia ya haja kubwa au puru (rectum) ya mgonjwa kasha kuzungusha zungusha ili kufahamu kama tezi limevimba ama la na pia hali yake kama ni gumu kuliko kawaida ama lina utando na nyama laini.
  2. Kipimo cha damu cha Prostate-Specific Antigen (PSA): PSA husaidia kutofautisha kati ya saratani ya tezi dume na BPH. PSA ni aina ya protein inayozalishwa na seli za tezi dume na kiwango chake huongezeka iwapo kuna saratani ya tezi dume.
  3. Utrasound ya Puru (Rectal Ultrasound): Kipimo hiki hufanyika iwapo daktari atahisi kuwepo kwa saratani ya tezi dume badala ya BPH. Utrasound ya puru pamoja na kuonesha taswira ya tezi dume ilivyo, pia humuwezesha daktari kuchukua kinyama (biopsy) kwenye tezi dume kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kutofautisha kati ya saratani na BPH.
  4. Kiwango cha utokaji wa mkojo (Urine Flow Study): Ni kipimo kinachotumika kufahamu kasi ya utokaji wa mkojo. Mkojo unaotoka kwa kasi na kiwango kidogo huashiria kuwepo kwa BPH.
  5. Kipimo cha kuchunguza kibofu cha mkojo (Cystoscopy): Kipimo hiki husaidia kuweza kufahamu ukubwa wa tezi, sehemu tezi lilipobana njia ya mkojo na kiwango cha kubana huko. Aidha huwezesha pia kutambua hali ya kibofu cha mkojo ikoje.


Matibabu

Matibabu ya BPH yameganyika katika sehemu mbili, yale yanayofanywa kwa kutumia dawa na yale yanayofanywa kwa kutumia upasuaji mdogo. Aidha matibabu hufanywa kwa watu wenye BPH kubwa zaidi na dalili zinazowaletea usumbufu na kuathiri maisha yao, wakati wale wenye dalili ndogo ndogo hawalazimiki sana kuhitaji matibabu.

Matibabu kwa njia ya dawa
Dawa hizi hutumika kwa lengo la kulifanya tezi dume kusinyaa na kupungua ukubwa wake. Dawa hizo ni pamoja na


  • Finasteride na dutasteride ambazo huzuia uzalishajiwa homoni ya DHT. Matumizi ya dawa hizi husaidia kuzuia kukua na kuvimba kwa tezi dume au kulifanya tezi dume kusinyaa kabisa kwa baadhi ya wanaume.
  • Terazosin, doxazosin, tamsulosin na alfuzosin husaidia kulainisha misuli ya tezi dume na hivyo kupunguza mbano wa mrija wa urethra, hali inayosaidia mkojo kutoka vizuri.



Matibabu kwa njia ya Upasuaji
Upasuaji mdogo (minimal Invasive procedures)

Upasuaji mdogo husaidia kuondoa dalili za BPH na hufanyika pale ambapo matibabu kwa njia ya dawa yameshindwa kuonesha mafanikio yeyote. Njia hizo ni


  • Tiba ya kutumia mawimbi ya joto (Transurethral microwave procedures, TUMT): Tiba hii hutumia kifaa kinachotoa mawimbi ya joto (microwave) yanayochoma na kuharibu tishu zilizovimba za tezi dume. Matibabu huchukua chini ya saa moja na yanaweza kufanyika bila mgonjwa kuhitaji kulazwa.
  • Tiba ya kutumia sindano maalum (Transurethral needle ablation, TUNA): Njia hii hutumia visindano vidogo ambavyo huunganiswa kwenye chombo chenye kutoa nishati ya joto kuunguza tishu zilizovimba za tezi dume.
  • Tiba ya kutumia joto la maji (Water-induced thermotherapy): Tiba hii hutumia maji ya moto yaliyochemshwa kwa kifaa maalum kuunguza na kupunguza tishu zilizovimba za tezi dume.


Upasuaji mkubwa

Madaktari wengi hushauri kuondolewa kabisa kwa tezi dume iwapo itathibitika kuwa mgonjwa ana BPH. Zipo njia nyingi za upasuaji wa BPH, nazo ni pamoja na upasuaji kwa kupitia kwenye mrija wa mkojo (Transurethral surgery, TURP), upasuaji mkubwa wa wazi (Open surgery), upasuaji wa kutumia nishati kuondoa tishu za tezi dume (Laser surgery), na upasuaji wa kutumia joto la fibreoptic probe kuchoma tishu za tezi dume (Interstitial laser coagulation).

Vitu vya kufanya baada ya Upasuaji wa Tezi dume
Mara baada ya upasuaji wa tezi dume inashauriwa 



  • Kunywa maji kwa wingi ili kusafisha kibofu cha mkojo
  • Epuka kujikakamua sana unapojihisi kwenda haja kubwa
  • Kula lishe bora ili kuepuka kupata choo kigumu. Iwapo mgonjwa atapatwa na choo kigumu ni vyema amuone daktari ili amshauri jinsi ya kuondoa tatizo.
  • Epuka na acha kunyanyua vitu vizito.
  • Hairuhusiwi kuendesha gari wala kuendesha mtambo wowote ule mpaka utakapopona kabisa.


Matatizo yanayoweza kutokea baada ya upasuaji


  • Shida wakati wa kukojoa: Kawaida huchukua muda wa siku kadhaa mtu kuweza kurejea katika hali yake ya kawaida ya kukojoa.
  • Shida ya kuthibiti mkojo usitoke ovyo (Incontinence): Ni kawaida kwa mgonjwa kushindwa kuthibiti kutoka kwa mkojo katika siku za mwanzo baada ya operesheni. Hata hivyo hali hii hujirekebisha baada ya siku kadhaa kupita.
  • Kutokwa na damu: Katika siku za wali mara baada ya TURP, kidonda kwenye tezi dume kinaweza kuvuja damu ambayo itaonekana katika mkojo. Hta hivyo hali hii hukoma baada ya wiki kadhaa. Hata hivyo iwapo utokaji damu ni mzito sana, inashauriwa kumuona daktari haraka.



Uwezo wa kufanya ngono baada ya upasuaji

Wagonjwa wengi waliofanyiwa upasuaji wa BPH uhofia sana kuhusu uwezo wao wa kufurahia tendo la ngono mara baada ya upasuaji. Kwa kawaida, huchukua muda fulani kwa agonjwa kuweza kurejea hali ya kawaida ya kufurahia tendo hili.


  • Mdiso au kudindisha (Erections): Madaktari wengi husema kuwa iwapo mgonjwa aliweza kupata mdiso au kudinda muda mfupi baada ya upasuaji, uwezo wake wa kuendelea kupa mdiso ni mkubwa zaidi. Hata hivyo iwapo mgonjwa hakuwa na uwezo wa kudisa tangu awali, upasuaji wa tezi dume hauna uwezo wa kumrejeshea uwezo wake wa kudisa.
  • Kutoa mbegu (Ejaculation): Ingawa wanaume waliofanyiwa upasuaji wa tezi dume bado wanaweza kupata mdiso, mara nyingi upasuaji huu huwafanya wawe wagumba yaani wasioweza kupata watoto. Hali hii kwa kitaalamu huitwa retrograde ejaculation au kilele (mshindo) kikavu (dry climax). Kwa kawaida, wakati wa tendo la ngono, mbegu za kiume kutoka kwenye korodani huingia kwenye urethra karibu na kijitundu cha kibofu cha mkojo. Wakati wa tendo la ngono, misuli maalum hufunga kijitundu hicho ili kuzuia mbegu zisiingie kwenye kibofu badala yake zielekee kwenye urethra ya katika uume. Hata hivyo, upasuajiwa BPH huondoa misuli hiyo na kufanya mbegu kuingia kwenye kibofu cha mkojo badala ya kuendelea kwenye urethra ya uume. Shahawa hizo hatimaye hutolewa nje ya kibofu pamoja na mkojo.
  • Kufika kilele (Orgasm): Huwa hakuna tofauti kubwa ya kufika kilele (orgasm) kabla na baada ya kufanyiwa upasuaji.


BPH na Saratani ya Tezi Dume: Hakuna Uhusiano wa moja kwa moja

Ingawa baadhi ya dalili za BPH zinafanan na zile za saratani ya tezi dume, kuwa na BPH hakuongezi uwezekano wa kupata saratani ya tezi dume. Hata hivyo, mwenye BPH anaweza pia na saratani ya tezi dume bila saratani hiyo kugundulika, ama wakati huo huo au siku za baadaye. Hivyo inashauriwa kuwa, ni vema wanaume wote kuanzia miaka 40 na keundelea kufanya uchunguzi wa tezi dume zao walau mara moja kila mwaka.

UTI NI UGONJWA WA HATARI UNAWEZA KUHARIBU FIGO.KIBOFU CHA MKOJO.


Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI) ni moja kati ya magonjwa ambayo hayapewi msisitizo wa kutosha katika jamii licha ya kuwa wengi huathirika kwa ugonjwa huu bila kujua chanzo, tiba na kinga yake.

Ugonjwa huu huanza kuathiri mirija inayopitisha mkojo, baadaye huenea katika kibofu na figo. Mgonjwa anaweza kupata ugonjwa sugu wa figo na kupoteza maisha kama ugonjwa huu hautatibiwa mapema.

Wataalamu wa afya wanasema UTI husababishwa na vimelea ambao huingia kupitia mirija inayosafirisha mkojo na kuutoa nje. Vimelea hawa wanashambulia kibofu na baadaye huendelea mpaka kwenye figo. Hii ndiyo hatua kubwa ya ugonjwa ambayo inaweza kusababisha kifo au tatizo la kudumu.

Hawa ni vimelea wa jamii ya bakteria walio wanajulikana kwa jina la escherichia coli (E.coli).

Bakteria hawa wanapatikana katika utumbo mpana lakini husafiri kupitia njia ya haja kubwa kwenda katika njia ya mkojo na kusababisha maambukizi katika kibofu na figo.

UTI inavyoenea

Dk Veronika Kaniki kutoka hospitali ya Sekou Toure, anabainisha tabia na mazingira yanayoweza kusababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuwa ni kushiriki ngono mara kwa mara na watu tofauti bila kutumia kinga.

Anasema hii inamfanya mtu kuchukua bakteria wa UTI kutoka kwa mwenzi wake ambaye tayari ana maambukizi hayo.

Dk Kaniki anaongeza kuwa kujitawaza kutoka nyuma kuja mbele baada ya haja kubwa kunapelekea maambukizi hasa kwa wanawake.

Hii ni kwa sababu vimelea hao hupatikana kwa wingi katika utumbo mpana.

Hivyo, kitendo cha kujisafisha kwa njia hiyo, anasema huwasafirisha bakteria hao kutoka sehemu ya haja kubwa kuja katika njia ya haja ndogo. Anasema mazingira haya husababisha UTI kwa wanawake kwa sababu njia ya haja kubwa na ndogo zipo karibu sana.
“Mama wajawazito pia wako hatarini zaidi kwa sababu mimba kukandamiza kibofu na kusababisha kukosekana kwa uwazi katika njia ya mkojo ambayo kitaalamu inajulikana kama incomplete emptying,” anafafanua Dk Kaniki.

Mtaalamu wa magonjwa ya figo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Fransis Fredrick anasema takwimu zinaonyesha kuwa kwa kila wanawake watano, mmoja amewahi kupata ugonjwa huo.

Hali hiyo anaielezea kuwa huweza kuwa ni ya kujirudia mara kwa mara kwa baadhi ya wanawake, hasa kinamama wajawazito na watu wenye umri mkubwa.

Mbali na wanawake kupata maambukizi zaidi, Dk Fredrick anaeleza kuwa watoto wa jinsi zote pia wako hatarini.

Anasema ni vema mazingira ya chooni na bafuni yawe safi ili kuwalinda watoto dhidi ya maambukizi haya.

Dk Fredrick anabainisha kuwa maambukizi katika njia ya mkojo yanaweza kusababishwa na bacteria, fangasi au virusi. Anasema matibabu yake hutolewa kulingana na aina ya vimelea waliosababisha maambukizi hayo.

Kisukari huathiri zaidi

Maambukizi haya yanaweza pia kuwaathiri watu wenye kisukari kirahisi zaidi kwa sababu ya sukari nyingi iliyopo katika mkojo.

Sukari hiyo huchochea kuzaliana kwa bacteria wanaosababisha maambukizi.

Kwa mujibu wa ripoti iliyofanywa na Chama cha Kisukari cha Marekani (ADA), asilimia 9.4 ya watu wanaokutwa na kisukari wanaugua pia UTI wakati asilimia 5.7 ni wenye maambukizi lakini hawana kisukari.

Wenye kisukari wanaathirika zaidi kwa sababu pia bakteria kuzaliana kwa wingi na baadhi ya mishipa inaharibika na kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo. Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa sukari nyingi iliyopo kwenye damu ya mgonjwa wa kisukari inaua seli nyeupe za damu, hivyo mwili unakosa kinga ya kupambana na bakteria hatarishi walioingia mwilini.


Athari, dalili, tiba

Dk Kaniki anafafanua kuwa endapo mtu hatatibiwa mapema au kumaliza dozi, ugonjwa huu unaweza kuwa sugu na kusababisha kuharibika kwa figo na kibofu.

Anasema maambukizi yanayotokea chini ya kibofu huathiri kibofu na mirija inayotoa mkojo nje.

Maambukizi yanayotokea katika figo ni hatua ya juu na athari zake ni kubwa zaidi kuliko athari zitokeazo katika mirija na kibofu.

Alibainisha athari nyingine kuwa mwanamke mjamzito anaweza kuzaa mtoto kabla ya wakati au mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu.

Anasema wagonjwa wanashauriwa kupata tiba mapema na kumaliza dozi na kwamba watoto wadogo na wazee pia wanaweza kupata maambukizi hayo kirahisi.

Ripoti ya ADA inabainisha dalili za awali kwa mtu mwenye maambukizi katika njia ya mkojo ni maumivu wakati wa kukojoa, kuhisi kukojoa laini ukienda chooni mkojo unatoka kidogo sana, kukojoa mkojo wenye damu na maumivu ya tumbo na mgongo.

Dalili kwa maambukizi yaliyokomaa, zinaelezwa kuwa ni homa kali, kutetemeka, kutapika, kuharisha na maumivu ya mgongo.

Hata hivyo, kinga ya ugonjwa huu inaelezwa kuwa ni kuzingatia kanuni za usafi hasa baada ya haja kubwa na kujisafisha kuanzia sehemu ya mbele kwenda nyuma ili kutoruhusu vimelea kuingia katika njia ya mkojo kwa urahisi.

Inashauriwa kumwona daktari baada ya kuona dalili hizi na kutumia kikamilifu dawa itakayopendekezwa na daktari.


Ni muhimu kwa mgonjwa kumaliza dawa ili kuzuia kujirudia kwa ugonjwa huo mara kwa mara na kusababisha madhara au usugu

FIGO KUSHINDWA KUFANYA KAZI (RENAL/KIDNEY FAILURE)




Figo ni miongoni mwa viungo muhimu sana katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu. Kwa kawaida, mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana kama yale ya maharage, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu za chini. 



Kazi za figo


Kazi kuu za figo ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu kadhaa katika damu na hivyo kusaidia katika kuhifadhi na kuthibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini. Katika kutekeleza hayo, figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika. 



Kazi nyingine za mafigo ni

  • Kurekebisha na kuthibiti kiasi cha vitu mbalimbali katika damu pamoja na kiasi cha maji katika mwili
  • Husaidia kutengeneza kiasili cha erythropoietin ambacho ni muhimu sana katika utengenezaji wa chembe nyekundu za damu.
  • Husaidia uzalishaji wa vitamini D
  • Husaidia pia katika kuthibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure)


Utengenezaji wa mkojo



Kwa kawaida damu inayozunguka mwilini hatimaye huingia kwenye figo kwa ajili ya kuchujwa, kutoa uchafu pamoja na sumu nyingine zisizohitajika mwilini. Kitendo hiki cha utengenezaji mkojo hufanyika katika hatua kuu zifuatazo;



  • Hatua ya kwanza ni uchujaji. Damu kutoka nje huingia ndani ya mafigo na kupita kwenye glomeruli, lenye umbo kama chekeche/chujio ambalo limeundwa na mishipa mingi midogo ya damu iliyojizungusha pamoja. Vitu mbali mbali, maji pamoja na sumu zilizo katika damu inayopita kwenye vimishipa hivi na kisha kuingia katika mirija mingine mikubwa kwa ajili ya uchujaji zaidi. 
  • Mirija inayofuata huendelea kuchuja damu na kunyonya baadhi ya vitu vilivyo chujwa kimakosa kuvirudisha mwilini, mpaka kiasi sahihi cha uchafu kinachotakiwa kuchujwa kinapokuwa kimefikiwa. 
  • Mara baada ya mkojo kutengenezwa na kutolewa kwenye figo, husafiri kuingia kwenye kibofu cha mkojo kwa kupita kwenye mirija ijulikanayo kama ureta. Kutoka kwenye kibofu, mkojo hutolewa nje ya mwili kupitia kwenye mrija waurethra.

Figo kushindwa kufanya kazi (Renal Failure/ Kidney Failure)

Kushindwa kufanya kazi kwa figo hutokea iwapo sehemu ya figo au figo lote litapoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kutoka katika damu na kutengeneza mkojo. Kitendo hiki husababisha kusanyiko la uchafu pamoja na sumu kadhaa katika damu ambazo ni hatari kwa afya ya mhusika. 

Aina za figo kushindwa kufanya kazi

Figo kushindwa kufanya kazi kumeganyika katika makundi yafuatayo

  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF) au Acute Kidney Failure (AKF). 
  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa kiasi (Mild renal/kidney insufficiency)
  • Tatizo sugu la figo kushindwa kufanya kazi (Chronic renal failure) 


Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF) 

Hii ni hali inayotokea kwa ghafla, na kudumu kwa saa chache mpaka siku chini ya 14, na kusababisha ongezeko la kiwango cha creatinine na urea katika damu. Hali hii huwapata karibu asilimia 5% ya wagonjwa waliolazwa hospitali kwa sababu ya matatizo mbalimbali. Aidha hali hii hutokea zaidi kwa wagonjwa mahututi na wale wanaohitaji uangalizi wa kipekee, yaani waliolazwa ICU


Katika makala hii tutatumia zaidi kifupisho cha ARF.


Visababishi na aina za ARF



Visababishi (au aina) vya ARF vinaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu:



  • Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal causes/failure
  • Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure
  • Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)



Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal 

causes/failure) 

Aina hii hutokea kwa takribani asilimia 60 mpaka 70 ya ARF zote. Katika kundi hili, figo hukosa damu ya kutosha kwa ajili ya kuchuja na hatimaye hushindwa kufanya kazi yake ipasavyo. Mambo yanayoweza kusababisha prerenal failure ni pamoja na:



  • Upungufu wa maji mwili unaosababishwa na kutapika kupita kiasi, kuharisha, au kupoteza damu kupita kiasi (kwa sababu ya ajali au kuumia) 
  • Kuvurugika kwa mtiririko wa damu inayoingia kwenye figo kwa sababu ya: 

    • Kushuka kwa ghafla kwa shinikizo la damu kwa sababu ya kupoteza damu nyingi wakati wa upasuaji mkubwa, kuumia au kuungua sehemu kubwa ya mwili, au maambukizi katika mfumo wa damu (sepsis) yanayoweza kufanya mishipa ya damu kutanuka na kushusha shinikizo la damu 
    • Kuziba au kusinyaa kwa mishipa inayopeleka damu kwenye figo 
    • Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) au shambulio la moyo (heart attack) linalosababisha kushuka kwashinikizo la damu 
    • Ini kushindwa kufanya kazi (liver failure) kunakoweza kusababisha mabadiliko katika mfumo wa homoni zinazoathiri shinikizo la damu pamoja na mtiririko wa damu kwenda kwenye figo.



Mwanzoni kabisa mwa pre-renal failure huwa hakuna athari yoyote inayotokea kwenye figo, na mara nyingi, figo laweza kurudi katika hali yake ya kawaida iwapo chanzo cha tatizo kitagunduliwa na kushughulikiwa ipasavyo. 



Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure) 



Mambo yanayosababisha madhara katika figo husababaisha karibu asilimia 25 mpaka 40 ya vyanzo vyote vya ARF. Visababishi vilivyo katika kundi hili hujumuisha vile vinavyoathiri uchujaji, mtiririko wa damu ndani ya figo na seli za figo zinazoshughulika na uchujaji na ufyonzaji wa chumvi na maji. 



Visababishi hivyo ni pamoja na:



  • Magonjwa katika mishipa ya damu 
  • Kuwepo kwa damu iliyoganda ndani ya mishipa ya damu inayopita katika figo 
  • Ajali/Kuharibika kwa tishu na seli za figo 
  • Magonjwa ya mzio katika glomeruli na figo kwa ujumla (glomerulonephritis). Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na maambukizi (infection) ya bacteria jamii ya streptococci. 
  • Magonjwa ya mzio katika nyama za figo (acute interstitial nepthritis). Mambo yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa kama vile Aspirin, Ibuprofen (Brufen), baadhi ya antibiotics, na baadhi ya dawa za kutoa maji mwilini (antidiuretics); magonjwa kama vile saratani ya damu (leukemia), lupus na lymphoma. Magonjwa ya mzio katika nyama za figo husababisha madhara katika seli zinazohusika na uchujaji na ufynzaji wa chumvi na maji. 
  • Magonjwa ya ukosefu wa damu katika mirija ya figo (acute tubular necrosis) ambayo hufanya seli na tishu za mirija hii kufa na hivyo mirija kushindwa kufyonza chumvi na maji kuyarudisha mwilini. Mambo yanayosababisha hali hii ni pamoja na shock (upungufu wa damu kuingia kwenye figo), matumizi ya madawa kama vile baadhi ya antibiotiki, sumu, dawa zinazotumika viwandani na kwenye x-rays na baadhi ya madawa yanayotumika kutibu saratani.




Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)



Mambo yanayosababisha hali hii huchangia kati ya silimia 5 mpaka 10 ya vyanzo vyote vya ARF. Postrenal failure wakati mwingine huitwa pia obstructive renal failure kwa sababu husababishwa na mambo yanayozuia utoaji wa mkojo nje ya figo. 



Kuziba kwa ureta moja ama zote mbili kunaweza kusababishwa na:



  • Vijiwe figo (renal stones) 
  • Saratani ya viungo vya njia ya mkojo au viungo vilivyo karibu na njia ya mkojo kiasi cha kuzuia mkojo kutoka nje ya figo 
  • Matumizi ya baadhi ya madawa



Kuziba kwa njia ya mkojo katika eneo la kibofu cha mkojo kunaweza kutokana na:







Tafsiri nyingine ya ARF



Wagonjwa wa ARF wanaweza kupata mkojo kidogo sana au wasipate kabisa., au wanaweza kuwa na ongezeko la creatinine kwa kasi ya kutisha au kwa kasi ndogo sana. Hali hizi zinaweza pia kutumika kutoa tafsiri nyingine ya maana ya ARF. 



Mtu anayetoa kiasi cha mkojo chini ya 400mL kwa siku hujulikana kama ana oliguria, na huchukuliwa kuwa ana hali mbaya ya kutoweza kupona. 



Mtu anayetoa mkojo chini ya 100mLkwa siku husemwa ana Anuria, ambayo kama imetokea ghafla, huashiria kuwepo kwa tatizo la kuziba kwa mirija inayotoa mkojo kwenye figo zote mbili, na mara niyingi hali hii ni ya hatari zaidi. Tafsiri hii husaidia sana katika kuamua aina ya matibabu na muda wa kumpatia mgonjwa matibabu ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kumpata. 



Dalili za ARF



Katika hatua za mwanzo mwanzo, baadhi ya waathirika wanaweza wasioneshe dalili zozote za tatizo hili. Dalili ni kama 



  • Kupungua kwa uzalishaji mkojo 
  • Kuvimba mwili 
  • Kupoteza umakini 
  • kuchanganyikiwa 
  • Uchovu 
  • Kulegea mwili 
  • Kichefuchefu na kutapika 
  • Kuharisha 
  • Maumivu ya tumbo 
  • Kuhisi ladha ya chuma na uchachu mdomoni
  • Na katika hatua za mwisho kabisa, mgonjwa anaweza kupata degedege na hatimaye kupoteza fahamu (coma).




Vipimo na uchunguzi



Kama ilivyoainishwa hapo juu kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza wasiwe na dalili zozote za tatizo hili. Hata wale wenye kuonesha dalili, zinaweza zisiwe mahsusi (non-specific). Uchunguzi wa mwili unaweza usioneshe tatizo lolote lile, au kukawa na dalili chache sana ambazo zinaweza zisimsaidie sana daktari kufikia uamuzi. 



Baadhi ya vipimo vinavyoweza kugundua uwepo wa ARF ni pamoja na



  • Kipimo cha utendaji kazi wa figo (Renal function tests) ambacho husaidia kuchunguza kiwango cha urea (blood urea nitrogen (BUN) katika damu. Aidha husaidia pia kuchunguza ongezeko la kiwango cha creatinine katika damu. 
  • Uchunguzi wa kiwango cha madini mbalimbali katika damu (blood electrolytes) 
  • Uchunguzi wa damu (Full Blood Picture): Husaidia kuonesha uwepo wa maambukizi ya bacteria na/au upungufu wa damu mwilini (anaemia) 
  • Kupima kiasi cha mkojo kinachotolewa na mgonjwa katika masaa 24 
  • Uchunguzi wa mkojo (Urine analysis): Rangi ya mkojo, kiasi cha electrolytes, uwepo wa usaha au damu au casts.
  • Ultrasound ya figo na kibofu cha mkojo 
  • Renal biopsy. 




Matibabu ya ARF



Matibabu ya ARF hutegemea kwanza chanzo chake na pili ukubwa wa tatizo. Kujua chanzo cha tatizo husaidia kufahamu ni aina gani ya matibabu yanayohitajika wakati kufahamu ukubwa wa tatizo huathiri uchaguzi wa aina ya matibabu na hata hitaji la kufanya dialysis. Hata hivyo inashauriwa sana kumpeleka mgonjwa kwa daktari bingwa wa magonjwa ya figo (nephrologist) kwa matibabu zaidi.



Kulingana na chanzo cha ARF, baadhi ya matibabu yanayoweza kufanyika, hutolewa yakiwa na lengo la:



  • Kurekebisha kiasi cha upotevu wa maji mwilini ambapo mgonjwa hupewa i.v fluids pamoja kurekebisha kiasi cha madini (electrolytes) kilichopotea 
  • Kupunguza au kuzuia ongezeko la maji kwa wagonjwa ambao figo zao zimeshindwa kabisa kutoa maji nje ya mwili 
  • Kuongeza uwezo wa moyo kufanya kazi vizuri au kuongeza shinikizo la damu husaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenda kwenye figo 
  • Kurekebisha kiasi cha madini mwilini kitendo ambacho husaidia mwili kufanya kazi zake vema 




Dialysis



Iwapo pamoja na matibabu hayo, figo za mgonjwa zinaendelea kudorora, mgonjwa hana budi kufanyiwa dialysis. Dialysis ni kitendo cha kutoa uchafu na maji yasiyohitajika katika damu. Kitendo hiki hufanywa kwa kupitia mishipa ya damu iliyo chini ya ngozi (hemodialysis) au kwa kupitia tumboni (peritoneal dialysis). Katika hemodialysis mirija hii huunganiswa kwenye mashine ambayo hufanya kazi kama figo. Damu kutoka kwa mgonjwa huingia katika mashine kisha huchujwa ili kuondoa sumu, uchafu pamoja na maji yasiyohitajika kabla ya kurejeshwa tena mwilini. 



Kitendo hiki hufanyika angalau mara mbili mpaka tatu kwa wiki, na kwa kiasi fulani ni ghali na si watu wote wa kipato cha chini wanaoweza kumudu gharama zake.



Katika peritoneal dialysis, uchafu pamoja na maji kutoka katika mzunguko wa damu huingia katika nafasi inayotenganisha tumbo na utando wake (peritoneal space), huchujwa kwenye utando huo kisha hutolewa kupitia sindano maalum (catheter ) iliyowekwa juu ya ngozi na kuingia ndani ya tumbo (peritoneal cavity).



Matarajio



Wagonjwa wengi wenye ARF hupona bila hata kuhitaji dialysis mara tu chanzo cha tatizo kinapogundulika na kushughuikiwa mapema. Hata hivyo wakati mwingine, pamoja na matibabu, baadhi ya figo hushindwa kurudia kufanya kazi kwa ufanisi wake wa awali. Watu kama hawa hawa wanahitaji kufuatiliwa kwa ukaribu na umakini mkubwa. 



Kinga ya ARF



Inashauriwa



  1. kufanya uchunguzi wa figo walau mara moja kila mwaka. Hii husaidia kuchunguza utendaji wa figo na hivyo kuepuka madhara kabla hayajatokea. 
  2. Kunywa maji kwa wingi ili kuyafanya mafigo yatende kazi zake kwa ufanisi.
  3. Kuepuka matumizi ya vitu ama madawa yanayoweza kuathiri nyama, seli au tishu za figo. Ni vema kutumia dawa pale tu unaposhauriwa na daktari.
  4. Watu wenye hatari ya kupata tatizo sugu la kushindwa kufanya kazi kwa figo (Chronic Renal Failure) wanashauriwa kufanya vipimo na cuhunguzi mara kwa mara
  5. Muone mtaalamu wa afya mara tu uonapo dalili za kuwepo kwa shida katika kukojoa au uonapo damu katika mkojo

MAWASILIANO.

MAWASILIANO. SIMU NO. +255 713 684 712 E-MAIL: healthylivingproduct6@gmail.com TUPO : KUNDUCHI BAHARI BEACH